Jumapili 19 Oktoba 2025 - 11:06
Sauti ya Umma wa Kiislamu katika kuliunga mkono taifa la Palestina lazima isalie ikisikika kwa nguvu

Hawza/ Hujjatul-Islam Sayyid Hasnain Abbas Gardizi, Mwenyekiti wa Baraza la Wanazuoni wa Madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s) nchini Pakistan, amesema kuwa mkataba wa hivi karibuni wa kusitisha mapigano kati ya utawala wa Kizayuni na Wapalestina hauimaanishi mwisho wa mapambano, wala kusahaulika kwa suala la Palestina, na kwamba uungaji mkono wa Umma wa Kiislamu kwa taifa la Palestina lazima udumu ukiwa imara na wenye nguvu daima.

Kwa mujibu wa kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam Gardizi alieleza kwamba kusitishwa kwa mapigano hakupaswi kutafsiriwa kama amani ya kudumu, bali ni nafasi ya kuimarisha msimamo wa haki na Wapalestina.

Akiendelea na hotuba yake, alilaani unafiki na ujanja unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel, akibainisha kuwa: “Israel ni nchi yenye rekodi kubwa zaidi ya uvunjaji wa makubaliano ya kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa. Historia yake imejaa udanganyifu, ukatili, na usaliti. Kwa hivyo, kusitisha mapigano kulikoafikiwa hivi karibuni kunaweza kuwa ni mbinu ya kisiasa tu ya kuzipumbaza fikra za ulimwengu.”

Mwenyekiti wa Baraza la Wanazuoni wa Ahlul-Bayt (a.s) Pakistan alisisitiza kuwa mataifa yalioidhinisha mkataba huo wa kusitisha mapigano yana jukumu kubwa, akisema:

“Ni wajibu wa serikali hizo kuilazimisha Israel iheshimu masharti ya makubaliano, na kuzitetea kwa dhati haki za kibinadamu na za kitaifa za wananchi wa Palestina.”

Aliongeza kwa kusisitiza kuwa: “Kusitishwa kwa mapigano hakuwezi na hakupaswi kusitisha mapambano au kulifuta suala la Palestina. Ukombozi wa Palestina na ulinzi wa Msikiti wa Al-Aqsa ni jambo la kiimani, kiakida, na la heshima kwa Umma wa Kiislamu. Kadiri Wapalestina wanavyonyimwa haki yao ya kujitawala na kuunda dola yao huru, mapambano dhidi ya ukaliaji na dhulma yataendelea.”

Hujjatul-Islam Gardizi aliongeza akisema: “Utawala wa Kizayuni wa Israel leo ni mfano wa wazi wa dhulma, mauaji ya halaiki, na ubeberu. Wakati umefika kwa dhamiri za ulimwengu kuamka. Nchi zinazodai kuwa watetezi wa haki za binadamu zinapaswa kuacha kuunga mkono madhalimu, na badala yake kuwa tiba kwa majeraha ya taifa la Palestina.”

Aidha, alitoa wito kwa Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na taasisi nyingine za kimataifa kuchukua hatua za haraka, madhubuti na za haki katika kutatua mizizi ya tatizo la Palestina, na kuachana na siasa za upendeleo na unafiki dhidi ya ukaliaji wa Israel.

Katika hitimisho, Hujjatul-Islam Sayyid Hasnain Abbas Gardizi alisisitiza kuwa: “Kulitetea taifa la Palestina si suala la kisiasa tu, bali ni ibada na jukumu la kiimani. Umma wa Kiislamu unapaswa kuhifadhi umoja na mshikamano, na kusimama thabiti dhidi ya madola dhalimu, huku ukitoa msaada wa amani, thabiti, na wa kweli kwa wanyonge duniani.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha